Mwanafunzi
aliyeongoza kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa
mwaka jana, Nyakaho Marungu akipongezwa na mama yake Celestina Maro,
nyumbani kwao Kitunda Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani huo.
Dar es Salaam.
Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kwa
asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo Makubwa Sasa (BRN),
lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe na za seminari
zimeendelea kuporomoka.
Katika
matokeo hayo, Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera,
iliyoanzishwa mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa
mafanikio baada ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa
shule zenye watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo
iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule
zilizoshika nafasi 10 za mwisho.
Matokeo hayo
ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa
Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10 za
kwanza ni za binafsi.
Akitangaza
matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani
huo ni wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247
waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia
58.25 ya waliofaulu mwaka 2013.
Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70.
Hata hivyo,
pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia 1.7) kufikia wastani wa ufaulu
kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi kwani ni asilimia kama moja na
ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina imani tutaifikia.”
Alisema
watahiniwa 297,365 waliandikishwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana
139,400 sawa na asilimia 46.88 na wavulana 157965 sawa na asilimia
53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa 244,902 ikilinganishwa na watahiniwa
367,163 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2013.
“Idadi ya
watahiniwa wa shule walioandikishwa kufanya mtihani huo ilipungua kwa
asilimia 33.3 ikilinganishwa na watahiniwa walioandikishwa mwaka 2013.”
“Mwaka 2012
kati ya watahiniwa 386,355 waliofanya mtihani wa kidato cha pili,
watahiniwa 136,243 walirudia kidato cha pili na watahiniwa 250,112
waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani
wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na kuongeza:
“Kati ya
watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne 2014,
watahiniwa 288,247 sawa na asilimia 96.93 walifanya mtihani na
watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07 hawakufanya mtihani kutokana na
sababu mbalimbali.”
Alisema
watahiniwa wa shule, kati ya watahiniwa 244,902 waliosajiliwa watahiniwa
244,410 sawa na asilimia 98.17 walifanya mtihani ambao wasichana
walikuwa ni 110,603 sawa na asilimia 98.13 na wavulana ni 129,807 sawa
na asilimia 98.19. Watahiniwa 4,492 sawa na asilimia 1.83 hawakufanya
mtihani.
Kwa upande
wa watahiniwa wa kujitegemea, alisema kati ya watahiniwa 52,463
waliosajiliwa, 47,837 ambao ni sawa na asilimia 91.18, walifanya mtihani
na ambao hawakufanya ni 4,626 sawa na asilimia 8.82.
Ufaulu wa masomo
Dk Msonde
alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya msingi umepanda
kati ya asilimia 1.28 na 11.22 ikilinganishwa na mwaka 2013.
“Ufaulu wa
juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili na asilimia 69.66 ya watahiniwa
wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu na ufaulu wa chini kabisa
ni ule wa somo la hisabati ambalo asilimia 19.58 ya watahiniwa wote
waliofanya somo hili wamefaulu.”
“Ufaulu
katika masomo ya sayansi yaani fizikia, kemia na baiolojia umeendelea
kuimarika kidogo kwa kulingana na ufaulu wa masomo hayo mwaka 2013,”
alisema.
Katika
matokeo hayo, ufaulu wa kila somo na asilimia katika mabano ni Kiswahili
(69.66), kemia (56.73), Kiingereza (55.10), baiolojia (48.30), fizikia
(46.71), jiografia (37.96), uraia (37.70), historia (37.41), biashara
(34.29), uhasibu (42.20) na hisabati (19.58).
Matokeo yaliyozuiwa, kufutwa
Dk Msonde
alisema baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 184 waliobainika kufanya
udanganyifu. Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, 128 ni
wa kujitegemea na 56 ni watahiniwa wa shule.
Alisema kati
ya watahiniwa hao, 128 wanatoka vituo viwili vya Kisesa mkoani Mwanza
na Ubago visiwani Zanzibar, huku wengine 56 wakitoka shule mbalimbali.
“Tumeagiza
mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika katika vituo
hivyo vya Kisesa na Ubago kwani udanganyifu uliofanyika ni karatasi moja
ya kujibia mtihani imeandikwa na watu watatu tofauti jambo ambalo
linaonyesha hakukuwa na umakini,” alisema.
Shule kongwe na za vipaji hoi
Shule za
vipaji kama Ilboru, Mzumbe, Msalato, Kilakala, Tabora Boys, Kibaha na
Tabora Girls na Shule kongwe zinazomilikiwa na Serikali kama Pugu,
Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania na Jangwani, kwa mara nyingine
zimeshindwa kufua dafu kwa shule za binafsi.
Katika
orodha ya shule 10 bora shule binafsi zilizotamba katika matokeo hayo ni
Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian Boys (Pwani), St.
Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls (Dar es Salaam),
Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa), Marian Girls
(Pwani) na Feza Boys (Dar es Salaam).
Shule 10 za
mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho (Pemba), Kwaluguru (Tanga), Relini
(Dar es Salaam), Mashindei (Tanga), Njelekela Islamic Seminari (Kigoma),
Vudee (Kilimanjaro), Mnazi (Tanga), Ruhembe (Morogoro) na Magoma
(Tanga).
Watahiniwa 10 bora kitaifa
Dk Msonde
aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa ni Nyakaho Marungu (Baobab),
Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam (Marian Boys), Fainess Mwakisimba
(St. Francis Girls), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya
(Marian Boys), Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile Jimmy
(Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis Girls) na Mahmoud Bakili (Feza
Boys).
Wasichana 10 bora kitaifa
Katika
matokeo hayo mwanafunzi bora kwa wasichana ni Nyakaho Marungu (Baobab),
aliyefuatiwa na Fainess Mwakisisimba (St. Francis Girls), Angel Mcharo
(St. Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St.
Francis Girls), Levina Ndamugoba (Msalato), Veronica Wambura (Canossa),
Sifaely Mtaita (St Maris Mazinde Juu), Catherine Ritte (St. Francis
Girls) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Wavulana 10 bora
Dk Msonde
alimtangaza kinara kwa wavulana kuwa ni Elton Jacob (Feza Boys)
akifuatiwa na Samwel Adam (Marian Boys), Mugisha Lukambuzi (Bendel
Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Mahmoud Bakili (Feza Boys), Amani
Andrea (Moshi Technical), Mahmoud Msangi, Elias Kalembo, Haji Gonga na
Kelvin Sessan wote kutoka Feza Boys.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Picha na Goodluck Eliona